Tuesday, April 25, 2017

HATA NYAKATI ZIWE NGUMU VIPI USIACHE WALA USIOGOPE KUMTOLEA MUNGU (SEHEMU YA II).

Posted by Savior Ministry at 9:28 PM 0 Comments


Mpendwa ninakusalimu katika Jina lipitalo majina yote, Yesu Kristo, Mwana wa Mungu Aliye Hai.

Huu ni mfululizo wa pili katika mfululizo wa masomo ambayo tulianza jana wenye kichwa kinachosema “HATA NYAKATI ZIWE NGUMU VIPI USIACHE WALA USIOGOPE KUMTOLEA MUNGU.”

Katika SEHEMU YA I tuliona jinsi ambavyo fedha huko Misri zilifeli au kwa maneno mengine ilifika mahali ambapo mfumo wa uchumi ambao ulikuwa unategemea fedha (yaani kuuza na kununua) ulishindwa.

Huo mfumo wa uchumi ulipofeli, Wamisri waliutumia mfumo wa kubadilishana mifugo yao ili waweze kupata chakula, lakini nao huo ulifeli.

Baadaye wakaanza kuitoa ardhi yao kwa ajili ya kupata chakula lakini nao ukafeli.

Ndipo Yusufu akaja na mfumo ambao baada ya huo kuingizwa kazini hatuoni ukishindwa tena.

Ulikuwa mfumo wa kupanda na kuvuna.

Walipewa mbegu za kupanda na wakaenda kuzipanda wakapewa sharti kuwa pale watakapovuna watampa Farao asilimia 20 ya walichovuna na hiyo asilimia 80 iliyobaki itakuwa yao kwa ajili ya mbegu na chakula.

Naamini kile walichompa Farao kilikuwa kodi na katika kile walichobaki nacho, mbegu ziliwahakikishia kuwa na kitu katika msimu uliyokuwa unakuja na chakula kiliweza kukutana na mahitaji yao ya wakati ule.

Nilianza hili somo na mfano wa hili jawabu la kiMungu ambalo lilitolewa na Mungu kwa mkono wa Yusufu kwa Wamisri kwa sababu kwenye Agano Jipya la Neema, utoaji unafananishwa na kupanda na kuvuna.

II Wakorintho 9: 6 – 11.

6  Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. 7 Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. 8 Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema; 9 kama ilivyoandikwa,
Ametapanya, amewapa maskini,
Haki yake yakaa milele.
10  Na yeye ampaye mbegu mwenye kupanda, na mkate uwe chakula, atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha, naye atayaongeza mazao ya haki yenu; 11 mkitajirishwa katika vitu vyote mpate kuwa na ukarimu wote, umpatiao Mungu shukrani kwa kazi yetu.

Katika hii mistari ambayo tumenukuu tunaanza kuona akisema apandaye haba atavuna haba naye apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu.

Hapa tunaona akifananisha utoaji na upandaji maana hiki kipande cha maandiko kinazungumzia utoaji.

Ili twende sawa lazima kuelewa haya maneno yalityotumika hapa ya ukarimu na uhaba.

Ukarimu na uhaba sio lazima imaanishe uwingi na uchache lakini kwa hakika inamaanisha ulinganifu wa kile ulichotoa kutegemeana na kiwango cha Baraka ambacho Mungu amekubariki.

Nitoe mfano.

Tuna watu wawili A na B na A anayo shilingi elfu kumi na B anayo laki moja.

Katika utoaji A akatoa shilingi elfu tano B akatoa shilingi elfu arobaini.

Ukiangalia uwingi na uchache B atakuwa ametoa zaidi ya A lakini ukiangalia ukarimu na uhaba, A ametoa zaidi ya B maana A ametoa asilimia 50 ya alicho nacho na B ametoa asilimia 40 ya alicho nacho.

Mungu anapoangalia utoaji wetu ndicho anachoangalia.

Je tunatoa sawa na kiwango cha Baraka ambacho ametubariki nacho.

Kwenye maagano yote mawili makuu ya bibilia Mungu aliagiza watu watoe kwa kadiri ya kiwango cha Baraka alichowabariki nacho.

I Wakorintho 16: 1, 2.

1  Kwa habari ya ile changizo kwa ajili ya watakatifu, kama vile nilivyoamuru makanisa ya Galatia, nanyi fanyeni vivyo. 2 Siku ya kwanza ya juma kila mtu kwenu na aweke akiba kwake, kwa kadiri ya kufanikiwa kwake; ili kwamba michango isifanyike hapo nitakapokuja;

Hapa tunaona Wakorintho wakiagizwa watoe kwa kadiri ya kufanikiwa kwao.

Kwa hiyo haiwezekani sote tukatoa kwa kiasi na kiwango kile kile maana hatujafanikiwa kwa kiwango na kiasi kile kile.

Kumbukumbu la Torati 16: 17.

17 Kila mtu na atoe kama awezavyo, kwa kadiri ya baraka ya BWANA, Mungu wako, alivyokupa.

Unauona huu mstari?

Kila mmoja wetu anatakiwa atoe kama awezavyo.

Hakuna hata mmoja wetu mwenye udhuru wa kutokutoa.

Kila mmoja wetu atoe awezavyo, kwa kadiri ya Baraka ya Mungu aliyotupa.

Tunapoenda mbele za Mungu kutoa Mungu anajua amembariki na kumfanikisha kila mmoja wetu kwa kiwango gani na hicho ndicho kinachoamua tumetoa kwa ukarimu au uhaba.

II Korintho 8: 12.

12 Maana, kama nia ipo, hukubaliwa kwa kadiri ya alivyo navyo mtu, si kwa kadiri ya asivyo navyo.

Unaona kitu andiko hili linasema mtu wa Mungu?

Kama nia ya kutoa ipo mtu wa Mungu, hukubalika kwa kadiri ya ulivyo navyo na sio kwa kadiri ya usicho nacho.

Kwa hiyo ulicho nacho ndicho kinachoamua kiwango cha utoaji.

Kwa kuwa tumeona kuwa utoaji unafananishwa na upandaji na uvunaji, utakubaliana nami kuwa hakuna mkulima ambaye akishavuna anakula kwanza mavuno yake alafu kile kinachosalia ndicho anakipanda kwa ajili ya msimu ujao wa mavuno.

Yule mkulima kabla hajaanza kula mavuno yake anatenga kwanza atakachopanda na anachagua vizuri mbegu zake.

Kinachotumaliza sana kiuchumi ni kwamba Mungu huwa tunampa masalia baada ya kufanya matumizi yetu yote na tukiwa tunapita kwenye vipindi vigumu ndo mbaya zaidi.

Tunajikuta baada ya kutoa matumizi ya kwetu hakuna kinachobaki cha kumtolea Mungu.

Kumbuka kile Yusufu aliwaambia Wamisri.

Aliwaambia kuwa asilimia 20 wampe Farao alafu hiyo 80 iliyobaki ni yao kwa ajili ya mbegu na chakula.

Katika andiko ambalo tulilinukuu mwanzoni kabisa la I Korintho 9 tunaona maandiko yakituambia kwenye ule mstari wa saba kuwa kila mtu atende kama alivyokusudia moyoni mwake, lakini tukizingatia kile mstari wa 6 kimesema kuhusu uhaba na ukarimu, tusitoe kwa kulazimishwa wala kupangiwa, na wala tusitoe kwa huzuni maana Mungu hupenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu.

Ni muhumi sana moyo kukunjuka kabla mkono unaotoa haujakunjuka.

Alafu tunaona andiko likisema kuwa Yeye ampaye mbegu mwenye kupanda na mkate uwe chakula atatupa mbegu za kupanda na kuzizidisha.

Kinachozidishwa ni zile mbegu tunazopanda na katika muktadha ya hili andiko ni zile sadaka tunazotoa kwa kuzingatia kanuni ambazo tumetoka kuziangalia.

Utoaji una nguvu kiasi kwamba kupitia huo Mungu anatujaza kila neema kwa uwingi ili tuwe na riziki za kila namna siku zote na tuweze pia kuzidi sana katika kila tendo jema.

Unaweza kuona unapoacha kutoa kwa sababu kipindi unachopitia ni kigumu, kwanza unafunga majira ya kuvuna maishani mwako maana umefunga majira ya kupanda.

Unaona pia kuwa unazuia kupokea kila neema kwa uwingi kwa hiyo huwezi kuwa na riziki zote siku zote.

Unajikuta kwa sababu ya kuacha kumtolea Mungu inakata mtiririko wa kiMungu wa kukutana na mahitaji yako ya kila siku maana umejitoa kwenye hiyo kanuni kwa kuacha kutoa kwa hiyo kila siku unajikuta unastruggle kama wengine katika nyakati ngumu za kiuchumi.

Mtu wa Mungu hata upitie kipindi kigumu vipi kiuchumi usiache kutoa.

Endelea kuzingatia kanuni ya uhaba na ukarimu tuliyojifunza leo, endelea kutoa kwa kadiri ya kufanikiwa kwako na Baraka za Mungu maishani mwako ili uweze kuendelea kuvuna na kujazwa kila neema kwa uwingi ili usipungukiwe na riziki hata siku moja na uzidi sana katika kila tendo jema.

Mungu akubariki sana.
.

CARLOS RICKY WILSON KIRIMBAI.

WHATSAPP #: +255786312131.

Share This Post

Get Updates

Subscribe to our Mailing List. We'll never share your Email address.

0 comments:

The Savior Ministry Live Chat

© 2016 Savior Ministry.
Powered by Themes24x7 .
back to top